Serikali imesema imewarejesha kwenye orodha ya malipo watumishi 4380 walioondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara kimakosa wakati wa zoezi la uhakiki wa vyeti vya elimu na watumishi hewa nchini katika kipindi cha serikali ya awamu ya tano.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Deogratius Ndejembi ametoa kauli hiyo Bungeni Dodoma wakati wa kipindi cha maswali na majibu.
Naibu Waziri Ndejembi amesema idadi hiyo ya watumishi inajumuisha watendaji wa kata, watendaji wa vijiji, na watendaji wa mitaa wapatao 3,114.
Hivi karibuni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa aliagiza kurejeshwa kazini kwa watumishi wote walioondolewa kazini kimakosa na serikali kupitia msemaji wake Gerson Msigwa ikitolea ufafanuzi kuwa wanaotakiwa sio watumishi feki.