Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefungua Mkutano Mkuu wa 11 wa Kitaaluma wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania – TRAMPA, ambapo amewataka watunza kumbukumbu na nyaraka wazingatie miiko ya taaluma yao hususan utunzaji siri za Serikali na kufuata utaratibu rasmi wa utoaji taarifa.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Oktoba 27, 2023 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa TRAMPA katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza wadhibiti uvujaji wa siri za Serikali.

Amesema, “hakikisheni mnadhibiti matukio yanayokiuka taratibu ikiwemo kutumia mifumo rasmi katika kusafirisha na kutuma nyaraka badala ya kutumia njia zisizo sahihi. Ninasisitiza kila mmoja azingatie wajibu wa kutunza nyaraka na kudhibiti utupaji ovyo wa nyaraka na kusababisha kukutwa sokoni zikifungiwa bidhaa au kuachwa zikizagaa na kukutwa katika mikono isiyo sahihi.”

Waziri Mkuu pia amesema kila mtunza kumbukumbu awe msaada na mlinzi wa mwenzake ili kudhibiti upotevu wa nyaraka na majalada yenye taarifa muhimu. “Toeni taarifa kwa mamlaka kuhusu uwepo wa viashiria vya baadhi ya maafisa kumbukumbu wasio na maadili wanaosababisha upotevu wa nyaraka.”

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Maafisa Masuhuli wasimamie Ofisi za Masijala kwa kudhibiti vitendo vya kufanya ofisi hizo kuwa dampo au sehemu ya chakula. “Kila Afisa Masuhuli asimamie vizuri taratibu za kutunza au kuhifadhi nyaraka Pia yapo mazoea ya baadhi ya Viongozi kuzifanya Ofisi za Masijala kutumika kwa kula chakula. Ofisi ziwe na maeneo ya chakula.”

Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema katika kushughulikia changamoto za kiutumishi kwa kada hiyo, ofisi hiyo imekamilisha zoezi la kuhuisha Muundo wa Maendeleo ya Utumishi wa Kada ya Watunza Kumbukumbu na Nyaraka.

Tonali aziingiza vitani AC Milan, Newcastle Utd
Kishindo: Dkt. Tulia Akson aukwaa Urais