Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Kibaptista, Mchungaji Joseph Hayab amesema watu wasiofahamika wakiwa na silaha wameshambulia Kanisa hilo lililopo Bege kaskazini magharibi mwa Nigeria, na kuwateka nyara waumini 25 waliokuwa katika ibada ya Jumapili.
Shambulio hilo, ni utekaji wa hivi karibuni wa watu wengi nchini Nigeria, ambako ukosefu wa usalama ni moja ya changamoto kubwa zinazomkabili Rais mpya Bola Tinubu, ambaye anatarajiwa kuapishwa rasmi mwishoni mwa mwezi huu (Mei, 2023).
Mchungaji Hayab ambaye pia ni Mkuu wa chama cha Wakristo wa Nigeria katika jimbo la Kaduna, amesema Washambuliaji hao, walivamia kanisa hilo katika eneo la Chikun jimbo la Kaduna, ambapo awali waliwateka nyara watu 40, na watu 15 walifanikiwa kutoroka baadaye.
Msemaji wa Polisi wa Kaduna, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo bila kutoa maelezo zaidi ambapo hata hivyo, Magenge ya wahalifu wenye silaha nzito mara kwa mara huwateka nyara watu wengi kaskazini magharibi na katikati mwa Nigeria ili kulipwa fidia.