Jeshi la Polisi Nchini Tanzania limewakamata wafanyabiashara 11 na kuwafungulia mashtaka kuhusiana na tuhuma za utengenezaji wa jezi feki kwa msaada kutoka kwa viwanda vinavyotengeneza jezi hizo halisi.
Jeshi hilo limekamata feki za Simba 279 pamoja na watuhumiwa 15 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Tabora na Tunduma ambao walikutwa na jezi hizo wakiziuza.
Akizungumza jijini Dar es salaam jana Alhamis (Desemba 16), Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, amesema watu hao pia wamekamatwa na urembo wa shingo ‘SKAFU’ za jezi 300.
Misime amesema ufanyaji wa kosa hilo ni kuidhulumu serikali mapato kutokana na ukwepaji wa kulipa kodi wanaofanya.
“Kama inavyofahamika baadhi ya timu huingia mikataba na kampuni kwa ajili ya utengenezaji wa jezi kwa makubaliano rasmi na jezi zinapouzwa kiasi fulani cha fedha hupatiwa kwa ajili ya kulipa mishahara ya wachezaji na huduma nyingine,” Misime alisema
Amewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa pale wanapoona jezi feki zinauzwa ili kukomesha tabia hiyo mara moja.