Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo ametangaza rasmi kuanza oparesheni ya kukamata watu wanaovaa nguo zisizo na heshima kulingana na maadili ya Tanzania na kuwafikisha mahakamani.
Mkumbo amesema hayo wakati akitoa taarifa ya Usalama kwa mwaka jana.
”Hizi nguo hazipendezi na si maadili yetu, mnaiga wenzenu wanaovaa kwa sababu ya hali ya hewa ya kwao sasa tunatangaza kuanza msako mwaka huu na tutakayemkamata tunamchukua hivyo hivyo hadi mahakamani bila kumpa nguo ya kujifunika ili ndugu zake wamuone’’. Amesema Mkumbo.
Mkumbo amefikia uamuzi huo kutokana na kuongezeka kwa matukio ya ubakaji na ulawiti tofauti na matukio mengine ambayo yamepungua kutoka na jitihada za jeshi la polisi.
Ambapo takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka 2016 matukio ya ubakaji yalikuwa 144 huku mwaka 2017 yameongezeka na kuwa 149, wakati matukio ya ulawiti kwa mwaka 2016 ni 58 na kuongezeka kwa mwaka 2017 na kuwa 62.
Hata hivyo amesema kuwa sababu kubwa ya kuongezeka kwa matukio hayo ni kutokana na mila potofu, imani za waganga wa kienjeji na ukosefu wa elimu.
Aidha amewataka watanzania kwa ujumla wafahamu kuwa makosa hayo hayafai na yana adhabu kubwa ya kifungo cha miaka 30 au cha maisha.