David Elwin Snow mwenye umri wa miaka 37 na kaka yake wanatuhumiwa kuvamia usiku katika kituo cha polisi eneo la Utah nchini Marekani na kuiba  baiskeli yake iliyokuwa inashikiliwa na jeshi hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kitengo hicho cha polisi, Snow na kaka yake walifika katika kituo hicho Disemba 18 mwaka jana, majira ya mchana, ambapo mtu mmoja alikuwa anashikiliwa na alikamatwa akiwa na baiskeli hiyo. Baiskeli hiyo iliwekwa kwenye chumba cha kuhifadhia vielelezo vya watuhumiwa.

Kwakuwa Snow alikuwa hajaripoti kuhusu kuibiwa baiskeli, polisi walimtaka kuonesha vielelezo vya umiliki wa baiskeli hiyo kabla ya kumkabidhi, lakini hakuweza kuviwasilisha wakati huo, imeripotiwa.

Snow na kaka yake aliyeambatana naye kituoni hapo wanadaiwa kuona eneo ambalo baiskeli yao ilikuwa imehifadhiwa. Polisi wamesema baadaye usiku wawili hao walirejea kituoni hapo kimyakimya kisha kuondoka na baiskeli hiyo.

Afisa wa polisi, Nisha King ameiambia Desert News kuwa hawakujua kama baiskeli hiyo imeibiwa hadi mtu aliyekuwa ameshikiliwa awali akiwa na baiskeli hiyo, alipowaeleza kuwa alisikia vishindo vya watu wawili usiku na kwamba wanaweza kuwa waliichukua.

Snow na kaka yake ambao walikutwa na baiskeli hiyo, walikamatwa na kushikiliwa na jeshi hilo kwa kosa la kuvunja na kuiba katika kituo cha polisi.

Magufuli atoa siku 7 kwa mawaziri
50 Cent awaka mrembo kuanika kwenye kitabu walichofanya faragha