Wawekezaji kutoka katika nchi za Norway na Sweden wapatao 100 wapo tayari kuja nchini kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo mafuta na gesi, viwanda vya mbolea, Nishati na Viwanda vya kusindika mazao ya kilimo.
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji ameyasema hayo alipokutana na balozi wa Norway nchini Tanzania na kumueleza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania walipokutana Leo Machi 7, 2022.
Dkt. Kijaji amemueleza balozi wa Norway kuwa nchi ya Tanzania imeboresha mazingira ya uwekezaji nchini kwa lengo la kuvutia wawekezaji na kuhakikisha kuwa wawekezaji waliopo wanafaidika na kupanua biashara zao.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefungua milango kwa wawekezaji kuja nchini Tanzania kuwekeza kwenye sekta mbalimbali hususani viwanda vya kuchakata bidhaa za kilimo, viwanda vya dawa na Vifaa tiba, Nishati na mbolea.
Aidha Dkt. Kijaji amesema kuwa nchi yetu inafanya kazi na sekta binafsi Kwa karibu Sana ndio maana Mhe. Rais Samia amekuwa nao katika Kila ziara Ili kuwajengea uwezo sekta binafsi kwani ndio injini ya uchumi wa nchi.
Naye balozi wa Norway nchini Tanzania Balozi Elisabeth Jacobsen Amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini Tanzania sambamba na maboresho makubwa yaliyofanyika na yanayoendelea ili kuhakikisha Mazingira ya uwekezaji na biashara yanakuwa rafiki.
Balozi Elisabeth amesema kuwa mazingira ya Uwekezaji nchini Tanzania yameboreshwa na hiyo ndio imewavutia zaidi nchi za ukanda wa Nordic kujipanga Kwa ajili ya kuwekeza nchini.