Wachezaji wa Young Africans Crispin Ngushi na Yusuph Athuman huenda wakatolewa wakati wa Dirisha Dogo la Usajili msimu huu 2022/23.

Wawili hao wamekua na wakati mgumu wa kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Young Africans, hali ambayo inahofiwa huenda wakapoteza sifa ya kuwa na kiwango bora na kushuka kwa uwezo wao wa kupambana.

Mbali na kukosa nafasi ya kucheza kiksi cha kwanza, Wachezaji wao pia wamekua wakiandamwa na majeraha ya mara kwa mara, hivyo kukosa nafasi wa kuwa na utimamu wa mwili sambamba na wenzao.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya Young Africans kimeeleza kuwa, Ngushi na Yusuph watapelekwa kwa mkopo katika klabu za Ligi Kuu wakati wa Dirisha Dogo la Usajili, na pendekezo hilo limepata Baraka za Benchi la Ufundi.

“Ngushi na Yusuph walipata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza mara chache sana tangu waliposajiliwa hapa, wameshindwa kabisa kuingia kwenye mfumo na kuaminiwa moja kwa moja na Benchi la Ufundi, hivyo njia sahihi ya kuendelea kulinda vipaji vyao ni kuwatoa kwa mkopo wakati wa Dirisha Dogo la Usajili.”

“Tayari Benchi la Ufundi limeshatoa Baraka zote za wawili hao kutolewa kwa mkopo na inaaminiwa wakiwa huko watakapokwenda, wataweza kucheza mara wa mara na huenda watakaporejea watakuwa sawa kwa ajili ya kuwania nafasi kwenye kikosi cha kwanza dhidi ya wachezaji wengine hapa.” kimeeleza chanzo hicho

Itakumbukwa kuwa Crispin Ngushi alisajiliwa Young Africans akitokea Mbeya Kwanza FC iliyoshiriki kwa mara ya Kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, huku Yusuph Athuman akisajiliwa Klabuni hapo mwanzoni mwa msimu wa 2020/21 akitokea Biashara United Mara.

Phiri, Chama waandaliwa kuivuruga Young Africans
Sure Boy aondoa mashaka kambini Young Africans