Kocha Mkuu wa Young Africans Cedric Kaze amethibitisha kuwasilisha mapendekezo ya usajili wa wachezaji wengine wawili katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili, ambacho kilianza rasmi juzi jumatano (Desemba 16).

Kaze emesema wachezaji hao ambao amependekeza wasajiliwe wanacheza nafasi za kiungo na mlinzi wa kati, huku upande wa safu ya ushambuliaji akiiongezea nguvu kwa kumsajili mshambuliaji kutoka nchini Burundi Saido Ntibanzokiza.

Kaze amesema usajili wa wachezaji hao wawili umezingatia mapungufu alioyaona kwenye kikosi chake tangu alipowasili nchini, ambapo amefanikiwa kuiongoza Young Africans pasina kupoteza mchezo hata mmoja.

“Hutakiwi kusajili kutokana na presha za mashabiki au viongozi, tunahitaji wachezaji ambao watasaidia timu kufikia malengo yetu, kama nilivyoeleza awali kwamba tunahitaji kupata watu ambao watatusaidia katika malengo yetu,” amesema Kaze.

Wakati huo huo taarifa zinaeleza kuwa mshambuliaji Ntibanzokiza, huenda akacheza kwa mara ya kwanza mchezo wa Ligi Kuu kesho Jumamosi dhidi ya Dodoma Jiji FC, baada ya usajili wake kuidhinishwa na Shirikisho la soka Tanzania TFF.

Mshambuliaji huyo alicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Singida United na kufunga mabao mawili kati ya matatu yaliyoipa ushindi Young Africans kwenye mchezo huo uliochezwa mjini Singida, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mpambano dhidi ya Dododma Jiji FC.

Deogratius Munish ‘Dida’ arudi Ligi Kuu
Lwanga amuengua Morrison kikosini Simba SC