Mabondia wawili wa Tanzania leo Jumanne (Mei 02) wanapanda ulingoni kurusha karata ya kwanza katika mashindano ya ngumi ya Ubingwa wa Dunia (IBA) yanayofanyika nchini Thailand.
Mashindano hayo yanashirikisha mabondia 539 kutoka mataifa 107, Tanzania inawakilishwa na mabondia wanne ambao ni Alex Isendi, Yusuph Changalawe, Kassim Mbundwike na Alex Sita.
Rais wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT), Lukelo Wililo, amesema katika mapambano hayo, Alex Isendi atacheza na Usmonov Bakhodur kutoka Tajikistan katika pambano la uzito wa kati huku Yusuph Changalawe akizichapa na Naveriani Otar raia wa Georgia, uzito wa juu.
Wililo amesema mabondia hao wapo tayari kucheza mapambano yao na kuwataka Watanzania kuwaombea wafanye vizuri.
Amesema washindi wa medali ya dhahabu watapata zawadi ya sh. milioni 470 huku mshindi medali ya fedha akizoa sh. 234, wakati mshindi wa medali ya shaba ataondoka na sh. milioni 16.
Bondia Yusuph Changalawe amesema amejipanga kumkabili vyema mpinzani wake na anaamini kwa kiwango cha juu alichonacho atapata ushindi.
“Nimejipanga kufanya vizuri baada ya kujiandaa kwa muda mrefu na ninatamani medali ya dhahabu ije Tanzania,” ametamba Changalawe
Changalawe anapanda ulingoni akiwa na kumbukumbu ya ya kushinda medali ya shaba katika michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika mwaka jana, nchini Uingereza alipomchakaza, Curlín Richardson wa visiwa vya Anguila.