Jeshi la Polisi Mkoani Songwe linawashikilia watuhumiwa wawili raia na mkazi wa Mpulungu Zambia (48) na Mtanzania mkazi wa Msongwa Tunduma (59) kwa kosa la kupatikana na kutengeneza Noti bandia 12 za nchi ya Zambia zenye thamani ya Kwacha 50.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, ACP Theopista Mallya amesema tukio hilo limetokea Septemba 19, 2023 mtaa wa Nazareth uliopo kata ya Mwakakati Wilayani Momba, ambapo watu hao waliokamatwa wote ni Wanaume.

Amesema, watuhumiwa hao pia walikamatwa na karatasi 10 zenye ukubwa wa A4 zikiwa zimechapishwa kwacha 50 kwa idadi ya noti 36 ikiwa ni pamoja na karatasi ya A4 moja iliyochapishwa noti 4 zenye thamani ya kwacha 100 ambazo zilikuwa na namba EJ.228951989, EJ.220684457 na E.J17714847.

Aidha, Kamanda Mallya ameongeza kuwa pia walikamatwa wakiwa na visu viwili kikubwa na kidogo cha kukunja pamoja na vitambulisho viwili vya Zambia vyenye namba Z.17714847 na Z.1600353 na kwamba tukio hilo linaashiria kitendo cha kujipatia kipato isivyo halali na Watuhumiwa hao watafikishwa Mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Hata hivyo, amesema Jeshi la Polisi mkoa linaendelea kufuatilia mtandao huo wa utengenezaji wa noti bandia, ili kuweza kuwabaini wahusika na kwamba linakemea vikali utengenezaji wa noti bandia na kuwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuwabaini wahusika.

Gamondi achukuwa tahadhari Mbarali
Shambulizi la wasiojulikana lauwa Wanajeshi 29 mpakani