Wachezaji Bruno Gomes na Abdulmajid Mangalo huenda wakauwahi mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC utakaopigwa Disemba 02.
Wachezaji hao wa Singida Big Stars, hawakuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kilichocheza dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, na kushuhudia wageni wakiibuka na ushindi wa bao 1-0.
Daktari wa timu hiyo, Shaban Shija amesema maendelezo yao sio mabaya na kuanzia wiki inayofuata watakuwa fiti kucheza hivyo mashabiki wasiwe na hofu.
“Baada ya mchezo wetu dihidi ya Young Africans, Bruno alipatwa na tatizo kidogo kwenye mapafu huku Mangalo yeye ana shida kwenye misuli ya goti ingawa afya zao zinazidi kuimarika,” amesema Shija.
Shija ameongeza kuwa hadi kufikia mchezo wao dhidi ya Namungo FC utakaochezwa nyumbani kwao kwenye Uwanja wa Liti, Singida huenda mastaa hao wakawa fiti kwa asilimia 100 kucheza na kuisaidia timu.
Kwa upande wa kocha msaidizi wa timu hiyo, Mathias Lule amesema kwa jinsi ambavyo ligi hii imekuwa ngumu na yenye ushindani mkubwa unapomkosa hata mchezaji wako mmoja inakuwa ni pigo kubwa.
Bruno ambaye ni Raia wa Brazil anayeichezea Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu ambapo hadi sasa amefunga mabao matatu huku akiwa mchezaji muhimu katika kikosi cha kocha Van der Pluijm.