Watu wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mjini Zanzibar, baada ya kukamatwa na vipande 45 vya meno ya Tembo katika Nyumba ya kulala wageni iliyopo eneo la Fuoni kwa Mabata Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Akizungumza na Vyombo vya Habari, Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya jinai Visiwani Zanzibar, Zubeir Chembele amesema watu hao walikamatwa katika nyumba hiyo ya kulala wageni ya Fiori wakiwa katika hatua za mwisho za kibiashara.
Amesema, uchunguzi juu ya tukio hilo unaendelea na majina ya watuhumiwa hao kwa uchunguzi zaidi huku akisema watu hao mmoja ni mwenyeji wa Mkoa wa Kagera na mwingine ni mwenyeji wa Zanzibar.
Jeshi la Polisi Kamisheni ya Zanzibar, walipata taarifa kuhusu kuingizwa kwa meno ya tembo visiwani humo ambapo Polisi walishirikiana na kikosi kazi cha kupambana na ujangili cha Tanzania Bara – NTAP, na kufanikisha ukamataji.