Watu wawili wamefariki dunia na wanne wamejeruhiwa kufuatia kuporomoka kwa jengo la Beit Al Ajaib liliopo eneo la Forodhani Mjini Zanzibar jana Desemba 25.

Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Lela Muhamed Mussa kwa vyombo vya Habari, imeeleza kuwa jengo la Beit Al Ajaib liliporomoka sehemu ya mbele upande wa kulia wakati shughuli za kulifanyia matengenezo makubwa zikiendelea.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo matengenezo hayo yanafanywa na Mkandarasi kutoka nchi ya Italia aitwa Construzioni Generali Gilardi S.p.A (CGG), chini ya ufadhili wa Serikali ya Ufalme wa Oman kwa gharama ya Dola za Kimarekani takriban milioni 5.6.

Serikali imetoa pole kwa familia za wahanga wawili waliopoteza maisha kufuatia ajali hiyo ambapo maiti zao zilipatikana usiku wakati zoezi la uokozi lilipokuwa likiendelea.

Aidha, serikali inatoa pole kwa majeruhi wanne ambao ni wafanyakazi waliopata majeraha katika eneo la ajali na watu wote waliopata athari iliyosababishwa na kadhia hiyo.

Kufuatia taarifa hiyo, serikali imeahidi kuwa nao bega kwa bega katika kipindi hiki kigumu cha msiba na kuuguza na imewaomba Wazanzibari na Watanzania kwa jumla kuwa wavumilivu kwa kupoteza na kuuguliwa na wapendwa wao.

Aidha, serikali imetoa pole kwa kuathirika Nembo ya Urithi wa Dunia iliyomo ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar kutokana na kuporomoka sehemu ya mbele ya jengo la Beit Al Ajaib kama Urithi wa Dunia.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale imeamua kuunda Tume Maalum ya Uchunguzi kwa lengo la kuichunguza kadhia nzima ya kuporomoka kwa jengo la Beit Al Ajaib ili kubaini kila kilichotokea pamoja na kuishauri Serikali hatua mbali mbali zinazostahiki kuchukuliwa.

Aidha Serikali imeahidi kuwa itafanya jitihada zake zote ikiwa za binafsi ama kwa msaada wa wahisani kuhakikisha jengo la Beit Al Ajaib linarudi kama lilivyokuuwa na kuendelea kuwa Nembo ya Mji Mkongwe na Zanzibar.

Lissu atuma salamu
Mwili wa Mngereza kuagwa Jumanne Dar