Watu wawili wakazi wa Kijiji cha Busikimbi, Kata ya Maisome, Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza waliokuwa wakivua samaki ndani ya Ziwa Victoria wamepoteza maisha baada ya chombo walichokuwa wakitumia kuvulia samaki kukumbwa na dhoruba kisha kupinduka na kuzama.
Kaimu Ofisa Mtendaji, Kata ya Maisome, Revocatu Mchele amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea usiku wa kuamika Juni 8 mwaka 2022 saa tano usiku na kuwataja waliopoteza maisha kuwa Baraka Kazimili (24) pamoja na Shadrack Mbonabucha (22) wote wakazi wa Kijiji cha Busikimbi, Kata ya Maisome.
Amesema upepo mkali unaovuma ndani ya Ziwa Victoria kwa sasa unaweza kuleta madhara kwa wavuvi kama hawatachukuwa tahadhari zinatolewa na mamlaka ya hari ya hewa Tanzania juu ya uwepo wa kipindi cha upepo mkali utakaodumu hadi mwezi Agosti mwaka huu.
Mchele amesema hadi sasa miili ya watu hao haijapatikana na jitiahada za wananchi zinaendelea kuwatafuta.
Mmoja wa wakazi wa Kata ya Maisome, Tulubuza Galubundu amesema matukio haya ya watu kupoteza maisha wakivua samaki ndani ya ziwa kipindi cha kiangazi hutokea mara kwa mara hivyo elimu inatakiwa kutolewa kwa wavuvi ili kujikinga na hali hiyo.
Mkuu wa Wilaya Sengerema Senyi Ngaga amesema amepata taarifa juu ya tukio hilo na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linakwenda Kijiji cha Busikimbi, Kata ya Maisome kutafuta miili hiyo.
Ngaga ametoa rai kwa jamii ya wavuvi na watu wanaotumia mitumbwi kusafirisha abiria ndani ya Ziwa Victoria kuchukua tadhari wanapofanya shughuli zao ndani ya Ziwa Victoria.