Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaama linamtaka dereva wa gari aina ya Scania ambaye hajajulikana jina lake ajisalimishe haraka iwezekanavyo kituo chochote cha Polisi kilicho karibu na naye kujibu makosa yanayomkabili ya usalama barabarani ikiwemo kosa la kusababisha ajali.
Hayo yanajiri baada ya wanafunzi wawili kufariki dunia kwa kugongwa na gari aina ya Scania wakiwa stendi katika eneo la Afrikana barabara ya Bagamoyo Wilaya ya Kinondoni.
Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro ameeleza kuwa ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia Agosti 9 ambapo dereva alikimbia baada ya ajali hiyo kutokea.
“Wanafunzi waliofariki ni Collins Obed Ngowi (15) kidato cha pili Shule ya Sekondari Makongo na Salvina Otieno anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 10-15 mwanafunzi wa darasa saba Shule ya Msingi Mount Sery” amesema Muliro.
Kamanda Muliro amesema mwanafunzi mwingine aliyejulikana kwa jina la Ashura anayesoma kidato cha tano shule ya Sekondari Al-Haramain alipata majeraha katika sehemu za mwili wake ambapo aliwahishwa hospitali na kupata matibubu.
Aidha Kamanda amesema Jeshi la polisi linaendelea kuchunguza chanzo cha ajali hiyo pamoja na ukaguzi wa gari hilo.