Watu wawili wameripotiwa kuuawa kwa kuchomwa visu na mtu mmoja aliyekuwa akiwadhalilisha wanawake wa Kiislam katika treni ya abiria katika jiji la Portland, Marekani.

Kwa mujibu wa BBC, mtu huyo aliyekuwa kwenye treni hiyo alikuwa akitoa lugha za kichochezi dhidi ya waislam huku akiwaghasi wasichana wawili waliovaa kwa kujifunika vichwa vyao, akidai wanatakiwa kuuawa.

“Mtuhumiwa alikuwa kwenye treni na alikuwa akipayuka akieleza mambo mengi ikiwa ni pamoja na lugha za kichochezi dhidi ya waislam,” Sgt Pete Simpson aliwaambia waandishi wa habari.

Maneno hayo ya kichochezi na vitendo vya mtu huyo vilisababisha watu kadhaa kumfika kwa lengo la kumzuia, lakini alitoa kisu na kuwachoma vibaya wawili kati yao huku akimjeruhi mtu mwingine.

Kwa mujibu wa tamko la Jeshi la Polisi la Portland, kati ya watu walioshambuliwa mmoja alipoteza maisha papohapo na mwingine alipoteza maisha wakati akipewa matibabu hospitalini. Mtuhumiwa alikamatwa punde baada ya treni hiyo kusimama katika kituo kilichofuata.

Tume inayoshughulikia masuala ya uhusiano wa Kiislamu ndani ya Marekani umemtaka Rais Donald Trump kutoa tamko kulaani vitendo vya uchochezi dhidi ya waislam vinavyozidi kuongezeka. Tume hiyo ilisema vitendo hivyo pia vinachochewa na baadhi ya matamko ya Rais Trump na sera zake dhidi ya waumini wa dini ya Kiislam.

Hata hivyo, wasichana waliokuwa wakishambuliwa na mtu huyo walitoweka punde tu waliposhuka kwenye kituo husika. Lakini wazazi wao waliliambia gazeti moja la Oregon kuwa walikuwa wasichana wadogo, mmoja ni Mmarekani mweusi na mwingine muumini wa dini ya Kiislamu.

Magazeti ya Tanzania leo Mei 28, 2017
Chelsea, Arsenal kuonyeshana ubabe fainali ya kombe la FA