Serikali kupitia Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais ( Muungano na Mazingira), January Makamba, imetoa masharti sita kwa wazalishaji wa Pombe aina ya viroba wanayopaswa kuyafuata ikiwa wanataka kuendelea na biashara hiyo nchini, lengo la Serikali si kuwazuia wananchi kunywa pombe bila ni kuhakikisha wanakunywa pombe bora na iliyo na viwango.
Uamuzi huo wa serikali umetokana na kutangaza kupiga marufuku matumizi ya vifungashio vya plastiki vya pombe hiyo kuanzia Machi Mosi mwaka huu, huku akisema kwa watakaokaidi watakumbana na adhabu kali ya faini na vifungo gerezani.
Aliyataja baadhi ya masharti hayo ni pamoja na kuwa na barua ya ushahidi au barua kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwamba amelipa kodi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Cheti au barua kutoka mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kwamba mzalishaji amekuwa na kibali cha usalama wa kinywaji kwa miaka ambayo amekuwa anazalisha.
Kuwepo na cheti au barua kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwamba anauza bidhaa inayokidhi viwango.
Cheti cha tathmini ya athari ya mazingira (EIA) au ukaguzi wa mazingira (EA) kutoka Baraza la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) au ofisi ya Makamu wa Rais.
Ameeleza badala ya kutumia vifungashio vya plastiki sasa wazalishaji watapaswa kutumia chupa zenye ujazo wa mil.250 na si vinginevyo.
Pia alitoa tarehe maalumu ya waombaji kuwasilisha maombi ni kabla ya tarehe 28, febuari mwaka huu.