Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka Wazalishaji wa Vyakula vya Mifugo kupeleka sampuli za vyakula wanavyozalisha kwenye maabara ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania – TVLA, ili kuhakiki ubora na viwango kwa kuzingatia matakwa ya sheria kabla ya kuanza kuwauzia wafugaji Nchini au kusafirisha nje.
Wito huo ameutoa hii leo Septemba 29, 2023 wakati akifungua Warsha ya uzalishaji wa Protini kwa ajili ya Vyakula vya Mifugo na kupunguza ushindani, iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema, “Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetunga Sheria ya Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama (Sura Na.180) pamoja na Kanuni na Miongozo mbalimbali, lengo lake ni kuhakikisha vyakula vinavyozalishwa vinakidhi ubora na viwango stahiki, ili kuwezesha uzalishaji bora wa mifugo, samaki na mazao yatokanayo na mifugo na samaki.”
“Hivyo, ninapenda kupitia warsha hii kutoa rai na msisitizo mkubwa kwa wazalishaji wa vyakula vya mifugo wote nchini kuhakikisha wanapeleka sampuli za vyakula wanavyozalisha kwenye maabara ya TVLA ili kuhakiki ubora na viwango kwa kuzingatia matakwa ya sheria hiyo kabla ya kuanza kuwauzia wafugaji wetu au kuvisafirisha nje ya nchi,” alisisitiza Waziri Ulega.