Wazazi na Walezi, wameaswa kuwekeza nguvu kwenye malezi bora na elimu kwa Watoto, ili kukomesha vitendo vya ukatili na uhalifu katika jamii na Taifa na kutomfumbia macho yeyote atakayebainika kufanya vitendo vya ukatili kwa mtoto, kwani sheria zinaelekeza wazi juu ya adhabu ya vitendo vya kiuhalifu.
Rai hiyo imetolewa na Konstebo wa Jeshi la Polisi, Herieth Mbwana wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Malinyi wakati akitoa elimu Kijiji cha Nawigo kilichopo Wilayani Malinyi Mkoani Morogoro, kuhusu madhara ya ndoa za utotoni na kupinga vitendo vya ukatili.
Amesema, Dawati limekuwa ikipokea malalamiko mengi yanayohusisha ukatili huku baadhi ya wazazi wakihusishwa na vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na kukatisha ndoto za watoto kwa kuwaozesha wakiwa bado na umri mdogo na kuwanyima fursa ya kupata elimu.
Herieth amesema, ni wajibu wa kila mzazi na mlezi kutambua sheria zinazowalinda watoto katika makuzi yao kwa kutambua madhara ya ndoa za utotoni, mila potofu katika jamii na kufahamu ulinzi wa mtoto dhidi ya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.
Mmoja wa wazazi, Mama Rukia amesema wamekuwa wakiona aibu kuzungumza na watoto wao kuhusu vitendo hivyo, kutokana na mila na desturi ila elimu waliyoipata wanaamini italeta matokeo mazuri katika jamii zao kwa kuanza kuzungumza kwa pamoja kuhusu madhara yatokanayo na vitendo vya ukatili ili kuwalinda nakuwajengea uwezo wa kuzungumza na hasa watoto wa kike.