Jumuiya ya wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), imetakiwa kuendelea kuwajengea uwezo Viongozi wa Shule, ili heshima yao iendane na muda waliokaa kwa kipindi chote walichokuwepo katika maeneo yao ya kazi.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ameyasema hayo hii leo Julai 15, 2022, na kuongeza kuwa mpango wa chama hicho ni kuongeza tija katika kujenga mafanikio katika shule zinazomilikiwa na CCM.
Chongolo, ambaye alikuwa akifungua kikao cha Wakuu wa shule za Umoja wa Wazazi Tanzania, amesema lengo la CCM la kuanzisha shule ni kuwawezesha vijana kupata elimu bora ambapo kwa mwaka huu wamekuwa na ufaulu wa mitihani unaoridhisha.
“Katika matokeo ya mtihani mwaka huu karibu asilimia 80 hadi 90 ya wanafunzi wanaosoma katika shule zinazomilikiwa na chama wamepata ufaulu wa daraja la kwanza na la pili, ni mwanafunzi mmoja tu kapata ufaulu wa daraja la nne,” amesema Chongolo.
Aidha, amewasisitiza Wakuu wa shule kuendelea kujenga nidhamu katika maeneo yao ya kazi na kwa wanafunzi katika shule zao, hatua itakayosaidia kuendelea kujenga heshima ya chama na shule husika kwa minajili ya kufikia malengo waliyojiwekea.
Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo amesema heshima ya mwalimu ni kupata matokeo bora na kwamba katika muhula ujao wamepanga kutoa zawadi kulingana na kiwango cha ufaulu katika shule itakayofanya vyema hivyo ni jukumu la kila mwalimu kuweka mikakati itakayomsaidia kufikia mafanikio.
Awali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Edmund Mndolwa aliwataka watumishi katika taasisi za elimu zinazomilikiwa na CCM kuacha kujihusisha na mambo ya kisiasa na badala yake wajikite katika kutoa elimu iliyo bora.