Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Monduli, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Rashid Nchimbi amewaomba wazazi waliowapeleka watoto wao wenye walemavu katika kituo kiitwacho St. John Paul II Rehabilitation Centre kilichopo Wilayani humo kwa ajili ya huduma mbalimbali wakawaeleze wenzao mafanikio waliyoyapata kutokana na maendeleo ya watoto wao.

ASP. Nchimbi aliyasema hayo kituoni hapo, baada ya Jeshi la Polisi kupata nafasi ya kutoa elimu ya Ukatili wa Kijinsia kwa wazazi wa watoto hao ambao wengi wao ni kutoka Jamii ya Kimasai na kudai kuwa watoto wao wanapata matibabu, wanafanyiwa mazoezi, kupewa viungo bandia pamoja na elimu basi kwa mafanikio hayo wanatakiwa wafikishe taarifa hizo kwa ndugu, marafiki na majirani.

“Endapo mtatoa taarifa za mafanikio haya kwa wenzenu wenye matatizo kama hayo, nao watapata muamko na hatimaye kuleta watoto wao kituoni hapa,” alisema ASP. Nchimbi.

Kwa upande wake mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto Wilaya ya Monduli Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Jacqueline Uhwelo alisema kumekuwa na matukio ya vipigo tena hadharani toka kwa akina baba kuwashambulia wenza wao lakini kutokana na mila potofu inasababisha wanawake hao kutotoa taarifa Polisi.

“Baadhi ya akina mama wa Jamii ya Kimasai wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya Ukatili hasa vipigo lakini wakichinjiwa kondoo basi yanaisha, je mnadhani hizo mila potofu zitaisha lini?” Alihoji Jacqueline.

Naye Mratibu wa kituo hicho, Mireile Kapilima pamoja na kulishukuru Jeshi la Polisi wilaya ya Monduli kwa kutoa elimu hiyo lakini pia akaahidi kuandaa kikao kikubwa kitakachowajumuisha wadau mbalimbali likiwemo Jeshi la Polisi kwa nia ya kuelimisha zaidi.

Marekebisho Miundombinu: Wizara yatoa lita 14,500 za mafuta
Washauriwa kujadiliana utatuzi changamoto za familia