Wanafunzi 686, kati ya 2591 kutoka Halmashauri ya Mji wa Makambako, Mkoani Njombe bado hawajajiunga na kidato cha kwanza mwaka 2019 kitendo kilichomlazimu mkuu wa wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri kuliagiza Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji huo kuhakikisha wanafunzi hao wanaanza masomo.
Ameyasema hayo katika kikao cha Pili cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Makambako, ambapo Mkuu wa Wilaya hiyo amewataka Madiwani hao kuhakikisha wazazi wote ambao hawajawapeleka wanafunzi shuleni kwa kisingizio cha kukosa sare za shule wawapeleke watoto wao shuleni haraka iwezekanavyo.
Amesema kuwa mwanafunzi ambaye alikwama kwenda sekondari kwa sababu ya kukosa sare za shule ni lazima apelekwe akiwa na sare alizokuwa akizitumia kabla ya kufaulu kujiunga kidato cha kwanza yaani sare za elimu ya msingi.
kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, Hanana Mfikwa amesema kuwa wazazi wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwapeleka watoto shule watashughulikiwa kisheria.