Tangu kuteuliwa kwa Martha Karua kuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga Nchini Kenya, Mwanamama huyo amekua gumzo duniani kote ikiwafika Afrika ndio inamsemea kwa mazuri yake na kumuandaa kuwa Makamu wa Rais wa Kenya baada ya Agosti 9, 2022.
Wazazi wa kiongozi huyo wa chama cha Narc Kenya Martha Karua, Josephine Wanjiru na Jackson Karua wameonesha furaha zao kufuatia kutangazwa kwake kuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga katika Muungano wa Azimio One Kenya.
Wakizungumza katika mahojiano na Citizen TV, walidai kushtuka baada ya kujua kwamba binti yao ametajwa kuwa mgombea mwenza wakisema kuwa ni muujiza.
Mzee Karua alisema kuwa ana furaha isiyokuwa na kifani kwa sababu japo anamtambua binti yake kama mwanasiasa mahiri, hakutarajia angefikia ngazi za juu katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali.
“Nimefurahi sana kwa sababu sikutarajia jambo hili. Sikufikiria kwamba ningeona siku ambayo angekuwa mgombea mwenza: haijawahi kuniingia akilini na kama baba, namsifu Mungu kwa sababu ndiye aliyeumba. hivi ndivyo itakavyokuwa,” mzee Karua alisema.
Kwa upande wake mama yake Martha Karua, alisema alijawa na furaha alipopokea habari za kuteuliwa kwa bintiye. Alibainisha kuwa uamuzi wa Raila ulimfanya ajivunie kama mama na kuongeza kuwa mwanasiasa huyo mashuhuri amewainua wanawake wengi.
“Ninajisikia vizuri kwa sababu, kupitia kwake, Mungu ameniinua sio mimi tu bali wanawake wengine. Amekuwa mchapakazi na mkali tangu alipokuwa mdogo. Hakuwa mtu wa kufuata umati na alisimama kidete katika maamuzi yake,” alisema.
Wazazi wote wa Martha walimwombea dua za Mwenyezi Mungu amuongoze binti yao wa pili pamoja na Raila kuleta mabadiliko yanayohitajika nchini.
“Nafikiri kuwa nchi itakuwa bora chini ya uongozi wake kwa sababu najua yeye si mtu wa kuhurumia ufisadi, wala hapendi kukejeli wengine. Mikononi mwao, Kenya itakuwa salama,” mamake aliongeza.
Kaka yake Karua alimmiminia sifa na kusema: “Hatujawahi kusema atafikia kiwango hicho lakini Mungu ni mwenye neema na ninaamini akiwa mtu wa uadilifu ndivyo alivyo, atabadili mwenendo wa taifa, sina hata maneno,” alisema.
Wakati huo mwenyewe Martha Karua ameanza kuonesha mbio akiwaambia watu wa Mt Kenya kuwa hawatajutia kupigia kura mrengo huo kwani atahakikishia Mt Kenya kuwa wako salama ndani ya Azimio la Umoja.
Alisema atachapa kazi vilivyo kwa sababu huwa hacheki wala kucheza ikifika ni masaaa ya kazi.
“Kati ya team yetu na ile ingine, ni gani inaweza kutimiza ahadi? Unajua mimi sitingiziki, sichezi wala sicheki masaa ya kazi, mkiniona hapo mjue Kenya iko sawa,” alisema Karua.
Hayo yanajiri ikiwa utafiti umeonyesha kuwa muungano wa Karua na Raila sasa ni maarufu katika kinyang’anyiro cha kuingia Ikulu. Katika utafiti uliofanywa baada ya Ruto na Raila kuwateua wagombea wenza, Raila anaongoza na asilimia 39 huku akifuatiwa na DP Rut kwa asilimia 35.
Hata hivyo Raila alionekana kupata umaarufu baada ya kumteua Karua kama mgombea mwenza na kwa mara ya kwanza amempiku DP Ruto.
Raila na Karua watamenyana vikali na Naibu Rais William Ruto na Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua wa muungano wa Kenya Kwanza katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.