Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema Serikali inatumia fedha nyingi katika kuimarisha miundombinu ya wanafunzi kusoma ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule za Msingi na Sekondari hivyo wazazi wana wajibu wa kuhakikisha wanafunzi wanakwenda shule na kudhibiti utoro.
Senyamule ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Potea Wilayani Kondoa wakati wa ziara yake ya kukagua miundombinu ya madarasa, ambayo yamekamilika na kuwataka kutunza miundombinu hiyo inayogharimu Serikali fedha nyingi na kuwatumia mkutano huo wa hadhara kuwahimiza jamii kutowaficha majumbani watoto wenye changamoto ya ulemavu.
“Sote ni mashahidi wa mabadiliko haya katika sekta ya elimu, madarasa mazuri yamekamilika na nyinyi mmechangia hapa nguvu kazi yenu, wazazi tutimize wajibu wetu wa kuwapeleka watoto shule, maana ya madarasa haya ni kuchochea maendeleo na ufaulu,” amesema.
Aidha, Senyamule ameongeza kuwa, “watoto walemavu wana haki sawa na wengine, kuwaweka nyumbani ni kuwanyanyapaa na kuwanyima haki za msingi msifiche watoto, watoeni wapate haki yao ya msingi ya kupata elimu bure inayotolewa na Serikali na madarasa haya yaliyokamilika yana miundombinu rafiki kwa wenzetu wenye changamoto za ulemavu.”