Wazee wa klabu ya Young Africans wameungana na idara ya Habari na Mawasilino ya klabu hiyo, kwa kuonyesha kusikitishwa na matendo ya baadhi ya waamuzi wanaochezesha Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22.
Idara ya Habari na Mawasiliano inayoongozwa na Hassan Bumbuli akishirikiana na Haji Sunday Manara jana Jumanne (Februari 09) ilikutana na Waandishi wa Habari na kueleza masikitiko yao kwa baadhi ya waamuzi wa Ligi Kuu.
Leo Wazee wa klabu hiyo wamekutana na waandishi wa habari na kueleza namna walivyochoshwa na mwenendo wa baadhi ya waamuzi, kwa kusema hawaitendei haki timu yao.
Wamesema haikuwa dhamira yao kuongea na waandishi wa habari, lakini hawana budi kufanya hivyo ili kuweka mkazo uliotolewa jana na Idara yao ya Habari na Mawasilino.
“Sisi kama WAZEE tumechoshwa na mwenendo wa WAAMUZI na imetufanya tutoke mbele na kuliongelea hili kwani tunataka mpira uchezwe kwenye haki.”
“TFF ilitazame hili kwa umakini mkubwa kwa sababu hapa kuna makusudi yanafanywa ili kuziumiza baadhi ya klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ikiwemo klabu yetu ya Young Africans.”
“Ni aibu kwa mpira wetu kuendelea kupigiwa kelele kila siku juu ya makosa ya waamuzi, inasikitisha sana jamani, tunajua Waandishi nanyi mtatusaidia katika hili.” wamesema Wazee wa klabu ya Young Africans.
Licha ya kulalamikia waamuzi, bado Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 36 baada ya kucheza michezo 14, huku Simba SC iliyocheza michezo 15 ikiwa nafasi ya pili kwa kuwa na alama 31.