Naibu Waziri, OR-TAMISEMI, David Silinde amesema Serikali ya awamu ya sita imeamua kujenga hospitali katika Halmashauri za Wilaya 35 ambazo hazikuwa na huduma hiyo kwa Wilaya, ambapo katika Mkoa wa Ruvuma zipo Halmashauri tano.
Silinde ameyasema hayo, mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyempa nafasi kuongea mbele ya viongozi wa Mkoa, Wilaya na Watumishi wa Halmashauri ya Madaba Mkoani Ruvuma, wakati akiwakumbusha watumishi hao wajibu wa kikazi.
Amezitaja Halmashauri hizo kuwa ni Mbinga, Songea, Madaba, Nyasa na Namtumbo huku akisema, “Hizi zimeshaanza kujengwa nchi nzima na tumetenga shilingi bilioni 35 za kuendeleza ujenzi katika hospitali hizi.”
Aidha ameongeza kuwa, katika mwaka huu wa fedha zahanati 700 nchini zimetengewa shilingi milioni 50 kila moja, ili kumalizia ujenzi wake na kufafanua kwamba “Ni shilingi bilioni 35 nyingine, tunamshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za miradi ili itoe huduma kwa wananchi wetu.”
Kuhusu sekta ya elimu, Naibu Waziri Silinde amesema wanafunzi milioni 1.56 wamefanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu na kwamba wizara yake inatarajia wanafunzi zaidi ya milioni 1.2 watafaulu mtihani huo.