Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais) Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Simbachawene amefichua jinsi baadhi ya watumishi wanavyopata ukuu wa idara na vitengo kwenye halmashauri kwa michongo ya rushwa.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) na maofisa utumishi wa halmashauri za Tanzania Bara.

Simbachawene alisema baadhi ya maofisa utumishi wanapokea rushwa kati ya Sh5 milioni hadi Sh10 milioni ili watoe ukuu wa vitengo na idara na kuongeza kuwa,“Kwa maofisa utumishi huko kuna changamoto, rushwa ni nyingi”.

“Wako watumishi huko wilayani, wanatuambia kabisa, pale kwetu siwezi kuteuliwa hata kama nina sifa, labda mniteue ninyi moja kwa moja. Sasa sisi Wizara ya Utumishi hatuteui tu watu, kuna mamlaka za ajira, lazima zifanye michakato, lakini haifanyiki kwa sababu ya rushwa,” alisema Simbachawene.

Simbacahwene amesema kuwa kuna changamoto ya watumishi kukaimishwa madaraka kwa muda mrefu, hali inayosababishwa na baadhi ya maofisa utumishi wanaotaka kupatiwa rushwa ndipo wapendekeze watumishi wengine.

“Hamuanzishi mchakato kwa sababu rushwa imewajaa. Nayasema haya mimi ni mbunge miaka 20, ni Waziri niliyepita wizara nyingi, wengine mko nao huko, ni jamaa zetu, ni ndugu zetu,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuanzia sasa, wakibaini kuna mtumishi mwenye sifa lakini hajaanzishiwa mchakato au kupandishwa cheo, ofisa utumishi wa halmashauri husika ataliwa kichwa.

Waziri Simbacahwene aliwataka wabadilike na wafanye kazi kwa weledi nakuongeza kuwa “Jamani hii nchi tunaiua wenyewe, huko kwenye mitandao mnatupiga kweli wakati ninyi ndio waharibifu,”

Naye, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Hendry Mkunda alisema kwa sababu suala hilo limesemwa na mamlaka, inaonyesha mifumo ya taarifa za utumishi haiko sawa, jambo linalotoa mwanya wa upendeleo kufanyika.

“Upandishaji wa vyeo na mengine haufanyiki kwa sababu ya utashi tu wa mtu, kama kuna mwanya ndiyo kabisa. Lakini ninachokiona mimi kwa hili huenda mifumo sio rafiki inatoa mwanya,” alisema Mkunda.

Usajili wa Caicedo waibua vicheko London
Banda afunguka ishu ya Chippa United