Waziri wa Maji na Umwagilaji, Prof. Makame Mbarawa ameagiza jeshi la polisi kumshikilia kwa saa 24 Mkandarasi wa Kampuni ya Water and Earth Works Ltd (BWE ), Emmanuel Mzena anayesimamia mradi wa maji wa Bwawani mjini Makambako mkoani Njombe kutokana na kushindwa kutekeleza mradi huo kwa wakati.
Mbarawa amefikia uamuzi huo mjini Makambako mkoani Njombe mara baada ya kufika na kuutembelea mradi huo kujionea maendeleo ya mradi.
“Nataka watu wako waje kwenye site na wewe utakaa ndani kwa masaa 24, mpaka utakapoleta wafanyakazi hapa site, sitaki masihara katika ujenzi wa miradi yote, na ninyi makandarasi mpaka muwekwe ndani ndio mfanyekazi, mnajifanya mnajua sheria kumbe nyie ndio wezi wa serikali,”amesema Prof. Mbarawa
Aidha, amemtaka mkurugenzi wa mamlaka ya maji mjini Makambako kusimamia mradi huo kwa kuhakikisha Tanki la Maji la Mradi huo linajazwa maji na akishindwa naye atawekwa ndani.
Kwa upande wake, mkurugenzi wa mamlaka ya maji Mjini Makambako, Huseni Nyemba amesema kuwa kutokana na agizo la waziri tatizo hilo linafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo licha ya kuwa mradi huo unasimamiwa na mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Iringa (ILUWASA).
“Huu mradi ulikuwa kiu yetu lakini wananchi wanatakiwa waelewe mradi ule walioingia mkataba ni mamlaka ya maji mkoa wa Iringa na wenyewe ndio wapo kisheria na kiutaratibu wa kimkataba sisi mamlaka ya maji Makambako ni kama wanufaikaji baada ya mradi kukamilika, nashkuru leo waziri alipotoa maagizo ni kama ametupatia ufunguo,”amesema Nyemba
Mradi wa huo maji Bwawani ulianza mwaka 2017 na ulitakiwa kukamilika mwezi wa sita mwaka 2018 lakini mpaka sasa haujakamilika.