Mwenyekiti wa chama tawala nchini Zimbabwe cha Zanu-PF, Oppah Muchinguri – Kishiri amekanusha taarifa kuwa alikatika titi katika tukio la mlipuko wa bomu lililomlenga Rais Emmerson Mnangagwa kwenye mkutano wa hadhara.
News24 imeripoti kuwa Gazeti la Daily News la nchini humo liliandika kuwa Muchinguri-Kashiri alisafirishwa kwenda nchini Afrika Kusini akiwa pamoja na makamu wa rais Kembo Mohadi kwa ajili ya kupatiwa matibabu ikiwa ni pamoja na kufanyiwa upasuaji wa titi.
Daily News walidai kuwa Muchinguri-Kashiri aliathirika katika tukio hilo baya ambalo lilisababisha vifo vya watu wawili waliokuwa kwenye mkutano huo wa hadhara wa kampeni siku chache zilizopita.
Mwenyekiti huyo wa Zanu-PF ambaye pia anafanya kazi kama Waziri wa Mazingira na Maji, amekanusha taarifa hizo kupitia kwa mwandishi maarufu wa Zimbabwe, Hopewell Chin’ono ambaye ni mshindi wa tuzo za uandishi nchini humo.
Hopewell Chin’ono ameandika alichozungumza na waziri huyo kupitia ukurasa wake wa Facebook.
Chin’ono amelitaka gazeti hilo kuomba radhi na kuchapisha tena habari sahihi kuhusu tukio hilo, lakini Mhariri Mkuu wa gazeti hilo, Gift Phiri ameshikilia msimamo wake akidai kuwa taarifa hizo walizipata kutoka kwa chanzo cha kuaminika.
Akizungumzia tukio hilo akiwa ziarani nchini Tanzania wiki iliyopita, Rais Mnangagwa alisema kuwa mlipuko ulitokana na bomu la kurushwa kwa mkono.
Mnangagwa anasema anaamini bomu hilo lililenga kumuua lakini siku yake bado haijafika.
Vyombo vya usalama nchini Zimbabwe vimesema vinaendelea kufanya uchunguzi lakini havijaweka wazi kama kuna mtu yoyote anayeshikiliwa kutokana na tukio hilo.