Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amewasili mkoani Tabora kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia leo tarehe 25 Septemba 2023 na kupokea taarifa kuhusu hali ya upatikanaji wa Umeme, huku akitoa maelekezo kwa wasimamizi wa utekelezaji wa Mradi wa usambazaji wa umeme vijijini.
Mara baada ya kuwasili mkoani humo, Kapinga alipokelewa na mwenyeji wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Kenan Kihongosi, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Urambo na baadaye kupokea taarifa hiyo katika Ofisi za Shirika la Umeme Tanzania – TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini -REA.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri atazungumza na wananchi wa Wilaya ya Nzega, Uyui na Urambo pamoja na kuwasha umeme katika baadhi ya vijiji vya wilaya hizo.
Aidha, Naibu Waziri huyo wa Nishati, Judith leo Septemba 25, 2023 atawasha umeme katika kijiji cha Ikindwa (Bukene), kilichopo Wilayani Nzega pamoja na kuzungumza na wananchi.