Serikali nchini imeendelea kusisitiza na kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya gesi ili kupunguza na kuondoa uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti katika maeneo mbalimbali nchini.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ameyasema hayo jijini Dodoma Novemba 6, 2019 wakati akizungumza na washiriki wa taasisi mbalimbali nchini kwenye mkutano wa majadiliano yanayoendelea katika wiki ya asasi za kiraia (AZAKI).
Amesema kutokana na msisitizo huo tayari baadhi ya wananchi wameanza kujenga mazoea ya kutumia gesi na kufanikisha mpango wa kupunguza ukataji hovyo wa miti ambao huchangia kuharibu mazingira.
“Tumekuwa tukisisitiza matumizi ya gesi ili kupunguza uharibifu wa mazingira maana uharibifu huu hutokana na ukataji hovyo wa miti ambao hufanywa na baadhi ya watu na kutokana na hali ya uelimishaji tayari wananchi wameanza kuzoea matumizi ya gesi,” amebainisha Dkt. Kalemani.
Amesema Tanzania inarasimali kubwa ya gesi ingawa bado ugunduzi wa mafuta haujafanikiwa na kwamba Serikali inaendelea kufanya jitihada juu ya jambo hilo ili kuleta hamasa katika kukuza uchumi kwani nchi inataka watu wake kufaidi rasilimali zilizopo.
Akiongelea wiki ya asasi za kiraia (AZAKI) Waziri Kalemani amezitaka taasisi hizo kutoa taarifa sahihi na kwa wakati ili wananchi waweze kujua mambo mbalimbali yanayoendelea ikiwemo kupata takwimu halisi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Madini Stanislaus Nyongo amesema Serikali imejipanga kuanza kusafisha dhahabu nchini ili kuongeza thamani yake hali iatayosaidia kukuza pato la Taifa ikiwemo kuhifadhi fedha Benki kuu kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya kimaendeleo.
Amesema mbali na hatua hiyo pia wanatarajia kujenga kituo cha kuchakata dhahabu jijini Dodoma na mkoani Geita ambavyo kwa pamona vitatumika kusafisha dhahabu ili kuongeza thamani yake na kukuza uchumi wa Taifa.
“Kwasasa dhahabu inayopatikana ni asilimia 80 na wengi wanahitaji isafishwe hapa nchini ili kufikia asilimia 99.9 kitendo kitakachopelekea benki kuu ya Tanzania (BOT) iweze kupata fedha inayotokana na dhahabu hiyo,” amebainisha Waziri Nyongo.
Awali akiongea katika mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Haki Rasirimali Rachel Chagonja amesema jukwaa la uzinduaji linalenga kuendeleza mijadala katika sekta ya madini, mafuta na gesi asilia hapa nchini.
Maonesho ya wiki ya asasi za kiraia yameingia katika siku ta tatu sasa ambapo yalianza rasmi jumatatu ya wiki hii Novemba 4, 2019 baada ya kufunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kasim Majaliwa.