Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametoa onyo kali kwa waziri wake wa ulinzi Nosiviwe Mapisa – Nqakula na kusimamisha mshahara wake kwa miezi mitatu kwa kupeleka ujumbe nchini Zimbabwe kwa ndege ya jeshi la anga.
Taarifa kutoka ofisi ya rais Ramaphosa imeeleza kuwa Chama cha upinzani cha Democratic Alliance kilikuwa kimemshutumu Mapisa-Nqakula kwa kutumia vibaya rasilimali za serikali kwa kuruhusu kundi kutoka katika chama tawala cha African National Congress (ANC), kusafiri naye hadi Harare mnamo mwezi Septemba.
Ofisi ya rais imesema kuwa Mapisa-Nqakula alikuwa katika ziara rasmi lakini uamuzi wake wa kuruhusu ujumbe ambao ulikuwa unasafiri kuelekea Zimbabwe kwa shughuli tofauti kuungana naye katika ndege hiyo ulikuwa ”kosa la kimaamuzi”.
Chama cha Democratic Alliance kimesema hatua iliyochukuliwa na rais Cyril Ramaphosa dhidi ya waziri wa ulinzi, Mapisa-Nqakula ni “kupigwa kofi mkononi”.
Msemaji wa wizara ya ulinzi hakujibu mara moja maombi ya kutaka maoni kutoka kwa waziri Mapisa-Nqakula ambaye mwenyewe pia hakujibu mara moja ujumbe uliotumwa kwenye mtandao wake wa LinkedIn.
Ramaphosa ameahidi kusafisha sifa ya chama cha ANC baada ya miaka kumi ya kashfa chini ya mtangulizi wake Jacob Zuma.