Denmark, Waziri wa uhamiaji na mwanachama wa chama cha Kiliberali, Inger Stojberg anayefahamika kwa mitazamo yake hasi dhidi ya uhamiaji amewatolea wito Waislamu kupumzika wakati wa Ramadhani akisema kufunga ni “hatari kwetu sote”.
Hayo yanakuja baada ya wiki iliyopita kuanza kwa mfungo wa Ramadhani ambao ni mwezi ambao Waislamu duniani kote wanafunga kuanzia alfajiri hadi jua linapozama.
“Natoa wito kwa Waislamu kuchukuwa likizo wakati wa Ramadhani ili kuepusha madhara kwa jamii nyingine ya Denmark,” Stojberg aliandika katika makala ya gazeti la udaku la BT.
“Nashangaa iwapo amri ya kidini inayoagiza kutekeleza nguzo ya miaka 1,400 ya Uislamu inawiana na jamii na soko la ajira tuliyonayo nchini Denmark mwaka 2018.”
Ameongezea kuwa anahofia kufunga kunaweza kuathiri “usalama na uzalishaji,” akitolea mfano wa madereva wa basi wanaoshinda bila kunywa au kula chochote kwa zaidi ya saa 10.
“Hii ni hatari kwetu sote,” amesema Inger Stojberg.