Watumishi watano wa Halmashauri ya Wilaya Kiteto mkoani Manyara wamesimamishwa kazi kutokana na kuisababishia hasara serikali.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa ameagiza kusimamishwa kazi na kuhojiwa na Taasisi Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) baada ya ziara yake mkoani Manyara.
Watumishi hao ni aliyekuwa Mweka Hazina Ndugu Nassoro P. Mkwanda na Mhasibu wa Mapato Ndugu Christopher G. Mwigani, Kaimu Mwanasheria wa Halmashauri Ndugu Joseph J. Hoza, Kaimu Mweka Hazina Ndugu Hadija Boffu pamoja na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi Nakaji Mollel.
Hata hivyo, Nassoro Mkwanda aliyehamishiwa Mafinga Mji, Khadija Bofu aliyehamishiwa Songea Manispaa na Christopher Mwigani ambaye amestasfu wote wanatuhumiwa kuhamisha fedha na kuweka kwenye akaunti ya amana isiyo na vifungu vya matumuzi na wanatakiwa kurejeshwa kwenye Halmashauri hiyo kujibu tuhuma hizo.
Naye Kaimu Mkuu wa kitengo cha manunuzi Nakaji Melateki Mollel aliidhinisha Sh. milioni 191.9 kwa ajili ya kununua vifaa vya ujenzi bila kufuata taratibu sambamba na Sh milioni 235.5 alizolipa mkandarasi wa kuchimba visima na Khalfan Hinga aliyetoa kazi hiyo bila kufanyika tathimini.
Pia amekemea tabia ya kuwahamisha watumishi waliofanya vibaya kwenye halmashauri na kusisitiza kuwa atawafuata popote walipo.
“Nilishakataza tabia ya mtumishi anafanya madudu halmashauri A na anahamishiwa halmashauri B, mtu akifanya madudu na kuhamishwa tutamfuata huko huko. Maelekezo ya CAG lazima yatekelezwe kwa mapana yake hawa watumishi wanatakiwa kuwa Takukuru wanachunguzwa. Hawa watumishi wafuatiliwe na sheria ichukue mkondo wake.
Bashungwa ametoa maagizo hayo wakati wa kuhitimisha ziara yake wilayani Kiteto mkoani Manyara kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.