Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro amelitaka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na wadau wa habari kupambana kwa hali na mali kubadili sheria za habari nchini.
Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo hivi karibuni jijini Arisha wakati alipokutana na uongozi wa TEF na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), na kuongeza kuwa wakati mzuri wa kulisukuma suala la kubadili sheria za habari ni sasa.
Amesema, “Rais Samia ameonyesha nia ya kutetea na kutoa haki za vyombo vya habari lisukumeni suala hili sheria zibadilishwe sasa, mkisubiri miaka 10 ijayo huwezi jua atakayekuja atakuwa na mtazamo gani juu ya vyombo vya habari.”
Aidha, amekubaiana na hoja ya TEF na wadau kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), kuwa na mamlaka ya kuwa mlalamikaji, mwendesha mashitaka, mtoa hukumu na msimamizi wa hukumu aliyoipitisha, ni kufifisha misingi ya utawala bora na sheria.
“Hili la utatuzi wa migogoro linahitaji uwazi kuna hatari kubwa katika kuweka madaraka yote kwenye chombo kimoja nafahamu sheria ililenga kuweka mlinganyo kwa maslahi yanayogongana, maana serikali zote duniani huwa zinawaza kudhibiti,” ameongeza Dkt. Ndumbaro.
Hata hivyo, amempongeza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kwa kuonesha nia ya kusimamia mabadiliko ya sheria hizo, na kuishauri TEF na wadau kuhakikisha wanakuwa karibu na Waziri Nape.
Vyombo vya habari, vipo katika mazungumzo na serikali kuomba Sheria ya Huduma za Habari, MSA 2016 irekebishwe katika vifungu vinavyofifisha Uhuru wa Vyombo vya Habari kikiwamo kifungu cha 9(a) kinachompa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) mamlaka ya kufungia vyombo vya habari bila kupitia utaratibu wa kuwasilisha malalamiko popote au pande zote mbili zilizo katika mgogoro kusikilizwa.
Sheria nyingine zinazolalamikiwa, ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018), kama zilivyorekebishwa mara kadhaa.