Waziri wa Maji Jumaa Aweso amewaonya  Wahandisi kuacha tabia ya uongo na kuwataka kuipa heshima taaluma yao kwa kutatua kero zinazowakabili wananchi pia amewataka watimize wajibu wao na kama wameshindwa kuendana na kasi yake waandike barua ya kuacha kazi.

Ameyasema hayo leo Juni 21,2021 wakati  akifungua mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma, kuzuia na kupambana na rushwa kwa Viongozi  wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) yaliyofanyika jijini Dodoma.

“Nilichokiona kwa Wahandisi wa maji ni uongo, uongo, uongo, huwezi kuwa Mhandisi wa maji muongo, unaitwa mtaalamu maana yake umesomea kitu kile unatakiwa kujibu kitaalamu lazima uheshimishe taaluma yako,” amesema Waziri Aweso.

Aidha Waziri Aweso amewataka  kufanya kazi na kuachana na visingizio visivyo na ulazima na kusisitiza kuwa kipimo kilichopo kwenye utendaji kazi wao ni kuona matokeo.

Hata hivyo Waziri Aweso amesema kuwa hivi karibuni anatarajia kutoa mkeka wa wahandisi kwa kuwafanyia mabadiliko wa RUWASA kwenda Mamlaka za maji na wa Mamlaka za maji kwenda RUWASA kwa lengo la kuleta ufanisi kwa wahandisi hao.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi  Clement Kivegalo, ameleza lengo la mafunzo hayo kuwa ni kuwaongezea uwezo Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji ili waweze kutimiza wajibu wao.

Pia amewaasa washiriki wa mafunzo hayo kuwa wasikivu  kwa kuwa lengo ni kuwaongezea uwezo kwenye utendaji kazi na kufikia malengo yaliyowekwa ya kufikia asilimia 85 ya wananchi vijijini wawe wanapata maji.

Nikki wa Pili: Nitaanza na vipaumbele hivi
RC Makalla atoa siku 2 wezi wa mafuta kujisalimisha