Waziri wa Maji Jumaa Aweso leo Novemba 20, 2021 amepita maeneo mbalimbali Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kujionea matokeo ya jitihada zilizofanyika kuhakikisha Maji ya Mto Ruvu yanakuja mitamboni baada ya kupambana dhidi ya uchepushaji unaotokana na shughuli za binadamu katika kukabiliana na changamoto ya maji iliyokuwa ikiwakabili Wananchi wa Dar es salaam ambao sasa wameanza kupata huduma.
Aidha Waziri Aweso ametembelea maeneo kama Sinza A, Manzese, Mabibo na maeneo mengine na kuahidi huduma kuimarika zaidi.
“Nimefungua mtambo wa tenki la Chuo Kikuu kuruhusu maji kwenda maeneo ya Survey, Masaki, Mikocheni, Kawe, Tageta, Mbweni, Makumbusho, Kijitonyama, Mwananyamala na Mjini Kati,” Amesema Waziri Aweso.
Ameongeza kuwa Novemba 19, 2021 kulifanyika zoezi la ufunguaji wa maji katika Bomba Kuu la usambazaji linaloelekea ukanda wa Magomeni baada ya kufungulia maji kutoka kwenye tenki ambapo huduma ya maji ilifika katika maeneo husika kwa muda wa saa 8 kuanzia saa 3 usiku ambayo ni Shekilango, Urafiki, Mabibo, Manzese, Sinza na Magomeni.
Halikadhali Waziri Aweso amethibitisha kupatikana kwa maji baada ya kukutana na wananchi waliomthibitishia kuwa maji kwenye maeneo Yao baada ya kukosekana kwa muda mrefu kutokana na kina Cha maji kwenye chanzo Cha maji kupunguza kiasi Cha kushindwa kusukuma maji kufika maeneo hisika.