Wizara ya Kilimo imegawa jumla ya lita laki moja za dawa ya kudhibiti viwavijeshi kwa wakulima wa maeneo yote yaliyoripotiwa kuwa na mlipuko wa viwavijeshi nchini.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Bwigili Kata ya Bwigili wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema serikali imechukua hatua hiyo ili kuwaepusha wakulima na hasara inayoweza kusababishwa na viwavijeshi.
Waziri Bashe amesema serikali inagawa dawa hizo bure na ameonya kuwa mtu yeyote asithubutu kuuza dawa zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya kugawiwa kwa wakulima kwani atachukiliwa hatua kali za kisheria.
“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inagawa dawa hizi bure katika maeneo yote yaliyoathiriwa na viwavi jeshi nchini, wananchi msikubali kuuziwa dawa hizi”.Amesisitiza Waziri Bashe.
Aidha Waziri Bashe amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Maafisa Kilimo kuhakikisha dawa hizo zinawafikia wakulima wote waliopatwa na mlipuko wa viwavijeshi.
Aidha Waziri Bashe ametoa wito kwa wakulima kushirikiana kutumia vifaa vya kunyunyizia dawa ili kuhakikisha kila shamba linahudumiwa ili lengo la serikali la kumuepusha mkulima na hasara litimie.
Hata hivyo Waziri Bashe amewaahidi wakulima kuwa katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2022/2023 serikali itatenga fedha kwa ajili ya kuwanunulia wakulima bomba za kunyunyizia dawa za kuua wadudu na kukabidhiwa kwa serikali za vijiji ili kuwasaidia wakulima, lakini pia amewakumbusha wakulima kutokuwa na haraka ya kuuza mahindi mara baada ya kuvuna kwani kuna uwezekano mkubwa wa kupata bei nzuri ya mazao ya chakula baada ya muda mfupi wa kipindi cha mavuno.
Kuhusu bei ya mbolea Waziri Bashe amesema serikali imepanga kutoa ruzuku ya mbolea ili kuwasaidia wakulima kupata mbolea kwa bei nafuu.
Akitoa shukrani kwa Mhe. Waziri, Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Living Kilawe amesema serikali imepeleka dawa hizo katika wakati sahihi na atahakikisha wakulima wanachanganya dawa na maji kwa kufuata vipimo sahihi ili kiangamiza viwavijeshi.