Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa ametoa wito kwa mikoa yote nchini kuiga Mkoa wa Mbeya katika kushirikiana na Wizara yake kuandaa Tuzo za Filamu katika miaka ijayo ili kukuza vipaji na kutoa ajira kwa wasanii wengi.
Bashungwa ametoa kauli katika kilele cha utoaji wa Tuzo za Filamu nchini iliyoratibiwa na Bodi ya Filamu chini ya usimamizi wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo.
“Ndugu yangu Comrade Juma Zuberi Homera, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, nakupongeza sana kwa kushirikiana na Bodi ya Filamu chini ya usimamizi wa wizara yangu.”amesema Bashungwa
Aidha amesema Serikali imeshatenga kiasi cha bilioni 1.5 kwenye mfuko wa Maendeleo ya Sanaa na Utamaduni kwa ajili kukuza na kuendeleza shughuli za Utamaduni na Sanaa ikiwa ni pamoja na Filamu.
“Ninawajulisha kuwa tuzo hizi ni endelevu, hivyo ninawakaribisha wadau wote wenye nia ya kushirikiana na Serikali kwa mwaka 2022.”
Katika Kilele hicho Rais Samia Suluhu Hassan amepewa tuzo ya heshima kwa mchango wake katika tasnia ya filamu nchini tuzo hiyo ilipokelewa kwa niaba yake na Waziri Innocent Bashungwa.