Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Innocent Bashungwa amewaomba mashabiki wa soka nchini pasina kujali itikadi zao, kujitokeza kwa wingi, Uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya jumamosi (Mei 22), kwa ajili ya kuipa nguvu Simba SC.

Simba SC ina kibarua kigumu cha kuhakikisha inafuzu hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kwa kuifunga Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini mabao matano kwa sifuri ama zaidi, katika mchezo huo wa Jumamosi.

Simba SC inadaiwa ushindi huo, kufuatia kufungwa mabao manne kwa sifuri katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliounguruma Jumamosi (Mei 15) mjini Johannesburg, Afrika Kusini.

Waziri Bashungwa ameliambia Bunge kuwa ushindi wa Simba SC ni ushindi wa Taifa, hivyo Serikali inaomba watu wengi kujitokeza kwa ajili ya kwenda kuishangilia timu hiyo.

“Niombe Watanzania wajitokeze kwa wingi kuishangilia timu ya Simba SC, tutambue kuwa timu inapocheza mchezo wa nje inawakilisha Taifa, Simba imekuwa ikifanya vizuri niombe tuwaunge mkono,” amesema Bashungwa.

Hata hivyo baada ya Waziri Bashungwa kutoa wito huo kwa mashabiki wa soka nchini kote, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu amesema majibu ya Waziri huyo, yawe kweli yanayotoka moyoni ili kuwe na mafanikio.

Inafahamika kuwa Waziri Bashungwa ni Mwanachama na Shabiki wa klabu ya Young Africans, ambayo ni mpinzani mkubwa wa Simba SC katika soka la Tanzania.

Kado aongezwa Timu ya Taifa
Lamine, Ninja waachwa Dar