Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum, Dkt. Dorothy Gwajima ameyataja mafanikio ya Wizara hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani na kusema Wizara yake imepata mafanikio yakupigiwa mfano.

Waziri Dkt. Gwajima, ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Machi, 28, 2022 kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Amesema Serikali ya Rais Samia, imewatambua rasmi Wamachinga kuwa Kundi Maalum ambapo tarehe 22-23 Februari 2022, Wizara iliandaa semina elekezi iliyofanyika Jijini Dodoma ikijumuisha viongozi 10 wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) ngazi ya Taifa pamoja na viongozi 78 kutoka Mikoa 26 ya Tanzania Bara.

“Kwenye kutekeleza ajenda ya haki za wanawake na usawa wa kijinsia na malengo ya jukwaa la kimataifa la kizazi chenye Usawa, tayari Mheshimiwa Rais Samia ameshaunda Kamati ya kitaifa ya ushauri  yenye Wajumbe 25 kutoka Pande mbili za Muungano (Tanzania Bara na Zanzibar) na kufanya uzinduzi jijini Dodoma  Desemba16, 2021” alisema Dkt. Gwajima

Aidha Serikali ndani ya mwaka mmoja tayari wamejenga Makao ya Taifa ya watoto yaliopo Kikombo Dodoma yenye thamani ya Shilingi Bilioni 12.7 ambapo jumla ya watoto 250 wanahudumiwa katika makao hayo, mafanikio mengine ni pamoja na kukabiliana na vitendo vya ukatili ambapo hadi kufikia Februari 2022, jumla ya Madawati saba (7) yameanzishwa katika Taasisi za Elimu saba (7) ambazo ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Iringa, Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Taasisi ya Ustawi wa Jamii na Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya cha Bugando.

Amefafanua kuwa katika kipindi cha Machi 2021 hadi Februari 2022, Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto 1,843 zimeanzishwa na kufanya idadi ya kamati za hizo kufikia 18,186 kati ya Kamati 20,750 zilizokusudiwa kuanzishwa kuanzia ngazi ya Kijiji/Mtaa hadi Taifa ifikapo Juni 2022

Katika hatua nyingine Dkt. Gwajima amesema katika kukabiliana na upungufu wa Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii Tasisi ya Manedeleo ya Jamii Kijitonyama, Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Vyuo vya Maendeleo ya  Jamii na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii Ufundi vimeendelea kutoa elimu kwa ngazi za Astashahada, Stashahada na Shahada ambapo Mwaka 2021/22, jumla ya wanafunzi 5,014 wa fani ya maendeleo ya jamii na wanafunzi 3,234 wa fani ya ustawi wa jamii walidahiliwa kwa mujibu wa vigezo vya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Mafanikio mengine yaliyopatikana ni kuhamashisha jamii katika ujenzi wa nyumba bora ambapo zimeongezeka kutoka nyumba 751 mwaka 2020 hadi kufikia nyumba 3,257 Februari 2022 ambapo nyumba hizo zilizojengwa Mikoa ya Arusha, Morogoro, Songwe, Shinyanga, Pwani, Katavi, Mtwara, Singida na Mwanza.

Akizidi kufafanua mafanikio hayo Dkt. Gwajima amesema, Wizara imeendelea kusimamia uanzishaji na uendeshaji wa huduma za vituo vya kulelea watoto wachanga na watoto wadogo mchana, ambapo katika kipindi cha Machi 2021 hadi Februari 2022, Wizara imefanikiwa kusajili vituo 303 vilivyodahili watoto 6,772 (Me 3,194 na Ke 3,578), vituo hivyo vimewezesha watoto kupatiwa huduma zinazochochea uchangamshi wa awali wa makuzi kimwili, kiakili, kihisia, kijamii na ukuaji wa lugha pamoja.

Sambamba na hayo yote Dkt. Gwajima, ametoa muelekeo wa bajeti ambapo amefafanua kuwa ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya Wizara, Serikali imewezesha kuongezeka kwa bajeti ya Wizara kutoka Shilingi 33,195,738,400 Bilioni, mwaka 2020/21 hadi Shilingi 43,625,929,000 Bilioni, mwaka 2021/22 ikiwa ni ongezeko la Shilingi 10,430,190,600 sawa na asilimia 31.

Davido anunua saa ya mkononi Bilioni 1.2
Tanzania na Liechtenstein kuwekeza kwenye kilimo