Makatibu wa afya nchini wametakiwa kusimamia nyenzo na rasilimali za kuendeshea huduma za afya zilizopo kwenye maeneo yao ya kazi kama ilivyo kwenye majukumu yao kwani wao ni kioo na alama ya uendeshaji wa taasisi.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa kufungua mkutano wa mwaka wa Chama Cha Makatibu wa Afya Tanzania ( AHSATA) unaofanyika mkoani Morogoro.

Dkt. Gwajima amesema Makatibu wa afya lazima waelewe vizuri majukumu yao ili kuweza kusimamia na kuendesha taasisi zao vizuri na hatimaye kupata mafanikio kwani wao ndio watendaji wakuu katika kusimamia mifumo ya afya .

“Tunataka mifumo imara ya afya na kuthamini jinsi Serikali ilivyowekeza kwenye mifumo hii ya afya” alisisitiza Dkt. Gwajima.

“Hata hivyo aliwataka makatibu hao kwenda kuisimamia kauli mbiu yao ya mwaka huu ambayo inasema, “Uimarishaji wa mifumo ya afya ni nguzo muhimu katika usimamizi wa rasilimali za sekta ya afya nchini” kuwa kutokana na kauli mbiu hiyo wanapaswa kuwajibika na kujiongezea thamani ya kazi zao wao wenyewe na kuweza kusimamia maslahi ya watumishi walio chini yao.

Aidha, Dkt. Gwajima amesema anatambua kada hiyo ndio pekee haina kurugenzi wizarani, hivyo kuagiza hilo lifanyiwe kazi ya uchambuzi kuona kuna kipingamizi gani kinachozuia hilo iwapo ni jambo lenye tija.

‘’Lazima tubadilike na tuondoe dhana ya uongozi kwenye afya lazima mtu awe kada ya utabibu ‘Medical Doctor andaeni kongamano litakalojadili hili,kwani mimi nilipokuwa DMO hata RMO nilifanikiwa kwa kusaidiwa na kada zingine,hivyo Muuguzi au taaluma nyingine ya afya anaweza kuongoza taasisi ya afya maana huo ni uongozi na siyo kazi ya taaluma maalumu’.

Aliongeza kuwa taasisi itakua na mafanikio endapo katibu wa afya atakua imara na taasisi haitofanikiwa endapo katibu wa afya atakua legelege hivyo lazima kada hiyo isimamie majukumu na kujiamini ili kuweza kuzifanya taasisi kuwa imara.

Pia Dkt. Gwajima amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwapatia fursa na uhuru wenye kuzingatia sheria makatibu wa afya ili kuweza kutekeleza majukumu yao.

Upande wa nidhamu, Waziri huyo aliwataka wanaporudi kwenye vituo vyao wakasimamie nidhamu kwani haitapendeza kuona taasisi wanazozisimamia zinafeli wakati wao ni watendaji wakuu ndani ya sekta ya afya.

Suala la Dawa na kadi za kliniki, Waziri huyo amesema anaona bado Kuna makosa yanaendelea kutokea licha ya kutoa tamko kwa baadhi ya vituo vya afya kuacha kuuza kadi hizo hivyo amewataka wasimamie hilo.

Awali akimkaribisha Waziri wa afya, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mh. Albinus Mugonya amewataka makatibu hao kuzingatia miongozo iliyopo katika utoaji wa huduma za afya zinazostahili na kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na ubunifu hivyo kutoa huduma bila upendeleo na kuwajibika kwa umma na kwa kuzingatia miiko na maadili ya taalumma zao.

Naye, Rais wa AHSATA Daniel Muhochi amesema katika mkutano huo watajadili na kubadilishana uzoefu na changamoto wanazokabiliana nazo na kutoka na njia ni namna gani wanaweza kuzitatua.

Muhochi aliomba ridhaa kwa wizara ili kada hiyo kuwa na baraza la taaluma litakalokuwa linashughulikia maadili kuweza kuboresha huduma za afya sehemu zao za kazi.

Viwanda vinaongeza dhamani
Ujenzi daraja la Tanzanite wafikia asilimia 83.5