Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia wanawake na makundi maalum Dk. Dorothy Gwajima, ametembelea kwenye kaburi alilozikwa mtoto Joseph Juma (4) ambaye alidaiwa kuuawa na Bibi yake Tatu Moshi (45) mkazi wa kijiji cha Lyabukande wilayani Shinyanga kwa kipigo na kumwagiwa maji ya moto. 

Waziri Gwajima ametembelea kaburi hilo akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali, pamoja na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, huku akifanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Lyabukande kukemea vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. 

Waziri Gwajima pamoja na viongozi wengine kwenye kaburi la mtoto Joseph

Alisema ameamua kufanya ziara mkoani Shinyanga, mara baada ya kusikia tukio hilo la mauaji ya mtoto huyo, pamoja na mdogo wake Limi Lameck mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi Saba, kujeruhiwa kwa kipigo na bibi yao, ambaye kwa sasa anapatiwa matibabu katika hospitali ya rufani mkoani humo ili kukemea vitendo hivyo vya ukatili. 

Waziri Gwajima na Mtoto Lameck

Aidha, aliitaka pia jamii wanapoona au kusikia mtoto wa jirani anafanyiwa vitendo vya ukatili, watoe taarifa mapema ili kudhibiti matukio hayo ambayo yamekuwa yakileta madhara na hata kusababisha mauaji. 

Alisema Sheria ya mtoto ya mwaka 2009 iliyofanyiwa marekebisho (2019) ina kataza mzazi kumuudhibu mtoto na kumsababishia madhara kwenye mwili wake, na kuwataka wazazi kuacha kutoa adhabu kali kwa watoto wao na hata kuwasababishia umauti. 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, alisema katika uchunguzi walioufanya walibaini pia watoto hao, walikuwa wakifungiwa ndani kila siku, wakati bibi na mama yao walipokuwa wakienda kutafuta riziki, lakini wana jamii walikuwa hawatoi taarifa na kufumbia macho vitendo hivyo. 


Aidha, alisema Serikali mkoani humo wanafanya utaratibu wa kutafuta mlezi ambaye atamlea mtoto huyo kwa muda, wakati mama yake akiendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi akiwa na bibi yao anaye tuhumiwa kusababisha mauaji, na kubainisha kuwa akikosekana mlezi ataendelea kuwa chini ya Serikali. 

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, aliwataka pia viongozi wa dini wakemee vitendo hivyo vya ukatili, pamoja na viongozi wa Sungusungu kuwa mstari wa mbele kupinga matukio hayo. 

Kwa upande wake Ofisa maendeleo ya jamii mkoani Shinyanga Tedson Ngwale ,alitaja takwimu za matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto mkoani humo, kuwa kuanzia mwaka 2021 hadi March 2022, kuwa kesi zilizolipotiwa 3,288, watoto wa kike 2625 na wakiume 663. 

Tukio hilo la mauaji ya mtoto huyo Joseph Juma( 4) pamoja na kujeruhiwa mdogo wake kwa kipigo na bibi yao, lilitokea April 18 mwaka huu majira ya saa 11 alfajiri, katika kijiji cha Lyabukande wilayani Shinyanga, kwa madai ya kujisaidia hovyo na Bibi huyo kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga pamoja na mama yao Herena Nicolaus. 

Njaa yasababisha mama amzike mwanae usiku wa manane
Kituo cha huduma za kibinadamu na operesheni za dharura cha Kanda kuanzishwa Nchini Msumbiji