Mbunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe ambaye ni Waziri wa Kilimo, Japhet Ngailonga Hasunga amesimikwa kuwa Chief Nzunda kutokana na majukumu makubwa anayoyafanya katika wizara yake sambamba na uwajibikaji uliotukuka katika Jimbo la Vwawa.
Hasunga amesimikwa kuwa Chief na Kiongozi wa Machief katika Wilaya ya Mbozi Chief Muleshwelwa Nzunda wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano uliofanyika Desemba 22, 2018 katika viwanja vya Stendi ya Maroli akiwa katika ziara ya siku tano ya kijimbo.
Sambamba na kusimikwa kuwa Chief Nzunda vilevile amekabidhiwa silaha za jadi ikiwemo mkuki wa kujilinda na maadui kutoka kwa Chifu huyo wa Mbozi.
Akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo, Mhe Hasunga amewashukuru wananchi hao kwa kumchagua kuwa mbunge wa Jimbo hilo katika uchaguzi wa Octoba 25, 2015 jambo lililompelekea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kumteua kuhudumu katika Wizara muhimu nchini ya Kilimo.
Amesema ushindi wake katika kiti cha ubunge ulisababishwa na imani kubwa ya wananchi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwani pamoja na changamoto mbalimbali ambazo zinaendelea kupatiwa ufumbuzi na serikali ya Awamu ya tano lakini CCM Pekee ndicho kitakachowaletea maendeleo ya Kijamii, Kiuchumi na Kisiasa hivyo wananchi wanapaswa kuendelea Kukiunga mkono.
“Huu ni muda wa kuungana na Rais katika kuhakikisha nchi inasonga Mbele kijamii na kiuchumi, Itikadi za kidini, Kisiasa na kikabila zinapaswa kuwekwa kando kwa maslahi mapana ya Taifa” Amesema Mhe Hasunga na kuongeza kuwa
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Taifa Mhe Dkt John Pombe Magufuli anatuhimiza kufanya kazi kwa bidii na hivyo ili kupambana vizuri katika hali zetu kiuchumi ni wazi kuwa lazima tukubali kuweka siasa kando”
Hasunga ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kufanya kazi kwa bidii kwani ndiyo silaha pekee ya maendeleo huku akisisitiza kuwa serikali inaendelea kuimarisha upatikanaji wa masoko ya mazao hivyo wakulima wanapaswa kuzalisha kwa bidii mazao mbalimbali ya kibiashara.
Aidha, ameahidi kuyafanyia kazi malalamiko ya wakulima kuhusu bei za pembejeo za kilimo ili kuwa na unafuu wa gharama zitakazoendana na uwezo wa wananchi.