Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo amemuagiza Afisa Elimu wa Mkoa wa Tabora kufanya tathmini ya haraka katika Shule ya Sekondari Isike ili funguliwe na kutumiwa na watoto wa eneo hilo.
Waziri Jafo ametoa agizo hilo leo bungeni alipokuwa akitoa majibu ya nyongeza katika maswali ya Mbunge wa Ulyankulu, Rehema Migilla ambaye ameiomba serikali kuifungua Shule hiyo kwa kuwa Shule ya Sekondari ya Ulyankulu imezidiwa wanafunzi huku wengine wakitembea umbali mrefu kwenda Shule ya Sekondari ya Mkindo.
Shule hiyo ilijengwa kwa ajili ya kuhudumia wakimbizi na jamii inayowazunguka lakini baada ya wakimbizi kurudi kwao na kubaki na wanafunzi wachache, serikali ililazimika kuwahamishia wanafunzi hao Shule ya Sekondari Ulyankulu.
“Jambo lako tumelichukua kwa kuwa tunafahamu eneo lile lilikuwa la wakambizi, na wewe ndio shuhuda kwenye eneo hilo hali ilivyo, hivyo namuagiza Afisa Elimu Mkoa wa Tabora aende kufanya tathmini ya haraka na kutoa majibu ya haraka ili kuwasaidia watoto wa eneo hilo.”amesema Waziri Jafo.
Awali, Naibu Waziri David Silinde amesema shule hiyo imefungwa kwa kuzingatia matumizi sahihi ya rasilimali watu, fedha na vifaa na kwamba serikali itafungua shule hiyo endapo itabainika kuna mahitaji.