Waziri wa (Tamisemi), Selemani Jafo ameagiza wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na wakuu wa shule kote nchini, kusafirisha wanafunzi waliokosa usafiri badala ya kuwaacha wakizagaa kwenye vituo vya mabasi.
Ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dodoma ambapo Machi 17, mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifunga shule zote za msingi na sekondari kwa siku 30 ili kuepusha kusambaa kwa virusi vya Corona mara baada ya Tanzania kuthibitisha kuwa na mgonjwa wa corona.
“Kama kuna shida wakuu wa shule wawasiliane na wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama ambao ni wakuu wa wilaya, haileti picha nzuri kuona wanafunzi wamezagaa vituoni wakitafuta usafiri jambo ambalo linadhihirisha kuwa wakuu wa shule hawakujipanga vizuri,” amesema Jafo
Amesema baadhi ya mikoa wanafunzi wameonekana kuzagaa na wengine kulala kwenye vituo vya mabasi kutokana na viongozi hao kutotekeleza agizo la kuhakikisha wanasafiri kwa usalama na amani hadi makwao.
Aidha ametoa pongezi kwa Mkuu wa Shule ya Kilakala iliyopo Morogoro na Mkuu wa Shule ya Dodoma Sekondari kwa kuweka utaratibu mzuri wa kusafirisha wanafunzi hao.