Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amesema kuwa UNICEF imekuwa na mchango mkubwa sana kwa kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukuza, kulinda na kutimiza haki za watoto.

Ameyasema hayo jana, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Shalini Bahuguna katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

“Kwa ujumla UNICEF imekuwa ikisaidia Tanzania kufanikisha agenda zake za maendeleo endelevu ya kulinda, kukuza na kutunza haki za watoto…..na tunaamini watoto hawa ni taifa la kesho,” Amesema Prof. Kabudi.

Waziri Kabudi amemueleza Bahuguna kuwa tangu mwaka 2016 Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na UNICEF, imefanikiwa kuboresha sekta za elimu na afya ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya upatikanaji wa huduma bora za kijamii, kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi na kuboresha huduma za maji katika mikoa mbalimbali ikiwemo, Dar es Salaam, Mbeya, Iringa, Kigoma, Njombe na Songwe.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini, Bahuguna amesema kuwa UNICEF itaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kulinda haki za watoto.

“Haki za watoto katika taifa ni jambo muhimu sana, hivyo UNICEF itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa haki za watoto zinalindwa pamoja na kupatiwa mahitaji muhimu,” Amesema Bahuguna.

Man Walter aanika madeni anayomdai Alikiba
Trump aapa tena juu ya Iran, aeleza athari za kipigo cha kulipa kisasi, Iran nao watoa taarifa yao