Waziri wa mambo ya nje, Prof. Palamagamba Kabudi leo Mei 9 amesema kuwa yeye pamoja na jopo la madaktari wamerejea nchini jana usiku kutoka nchini Madagascar wakiwa na dawa za kufanyia utafiti na siyo dawa ya kuanza kugawa kwa wananchi.
Prof. Kabudi amesema msaada wa dawa ambayo wamepewa ipo katika mfumo wa majani na dawa ya chupa ni mbili tu kwaajili ya marejeo ambapo wataalamu wa maabara watatafiti na kuchanganya ili kuweza kujua jinsi ya kuanza kutumiwa.
“Tumerudi kutoka Madagascar jana usiku ila hatujaja na dawa ya kuanza kugawa leo, tumekuja na dawa za kuanza utafiti na uchambuzi maabara, nimepokea simu nyingi, meseji WhatsApp Watu wanataka niwagaie, jamani sina dawa, sijaja na chupa za dawa”- amesema waziri Kabudi.
Na kuongeza kuwa “Chupa tumepewa mbili tu (control) ambazo zitasaidia pale wataalamu watakapochanganya dawa na kufanya utafiti na uchambuzi ili waone kama wamepatia, tumepewa wastani wa box 3 za dawa itakayotumika kama tiba na Box 8 za dawa itakayotumika kama kinga pale utafiti ukikamilika
Amesema wataalamu wa tafiti wa tanzania pamoja na wa madagascar wataendelea kushirikiana ili kuwezesha serikali kuona ni namna gani wataanza kutumia.
katika fomula waliyopewa aina ya majani amesema kuna ambayo itatengeneza dawa kwaajili ya wagonjwa na kuna ambayo itatengeneza dawa kwaajili ya kinga.
Aidha amebainisha kuwa endapo nchi yeyote ambayo itasema inadawa na ikawaita watanzania, serikali haitasita kwenda kuchukua na kufanyia utafiti.
“Madagascar wameijaribu wakajiridhisha kwamba ni salama ndiyo maana wanaitumia lakini sisi lazima tuifanyie utafiti na tujiridhishe kuwa inafaa, Ndege ya Rais haiwezi kuja na mzigo wa kutosha kugaiwa kwa Watanzania wote ,Nchi yoyote ikituita kwamba ina dawa tutaenda kuchukua” Amesema waziri Kabudi