Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji, Angellah Kairuka ameutaka uongozi wa kiwanda kinachotengeneza bidhaa za jasi (Gypsumboard) cha KNAUF kuendelea kushirikiana na jamii inayowazunguka katika kujiletee maendeleo.
Ameyasema hayo alipotembelea kiwanda hicho kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani ili kukagua shughuli za uzalishaji zinazoendela pamoja na kusikiliza changamoto za wawekezaji hao na kuweza kujadili masuala ya kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Amewataka kuona umuhimu wa kuchangia katika shughuli za kimaendeleo katika maeneo yanayozunguka kiwanda hicho hususani katika uboreshaji wa miundombinu na utoaji wa misaada itakayofikia jamii kwa sehemu kubwa na si mtu mmoja mmoja ili kuleta maendeleo katika eneo kubwa na kuondoa tofauti kubwa za kimaendeleo zisizoendana na maendeleo ya maeneo kiwanda hicho.
“Ni muhimu sana, na ni busara kuona ni kwa namna gani mnashirikiana na wananchi wanaozunguka eneo hili katika kuleta maendeleo ili kuhakikisha mnakubalika, na kuleta maendeleo ya eneo husika na kuondoa tofauti za kimaendeleo kati ya ustawi wa kiwanda na jamii inayowazunguka,”amesema Kairuki
Aidha, ameutaka uongozi huo kushiriki kimalilifu katika shughuli za maendeleo ikiwemo kuchangia kuboresha miundombinu inayozunguka mazingira ya kiwanda ili kuendelea kushiriki kwa vitendo na kuunga mkono jitihada za kuendelea eneo hilo.
Sambamba na hilo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Jumaa Abeld aliomba uongozi wa kiwanda kuona namna ya kuchangia katika maendeleo ya eneo lao kwa kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa sita katika shule ya msingi ya Kitangwi pamoja na madarasa manne katika shule ya msingi ya Kisemvule zilizopo Wialya ya Mkuranga katika mkoa huo.
Kwa upande wake Meneja Masoko wa Kiwanda hicho, Zainab Mwasara ameahidi kuwa ifikapo Julai 05 mwaka huu uongozi wa kiwanda utatoa taarifa za utekelezaji wa maombi hayo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 6.
Naye, Meneja Fedha wa kiwanda hicho, Wema Mboga ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya wawekezaji nchini na kupongeza ziara ya Waziri katika kutatua na kuahidi kufanyia kazi masuala yaliyoelezwa kuwa ni changamoto kiwandani hapo ikiwemo uhaba wa upatikanaji wa nishati ya umeme ya uhakika, kutokamilika kwa leseni za uchimbaji kwa wakati, tozo kubwa za malighafi na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji kiwandani hapo.